Saturday, 28 January 2017

MLAVIDAVI CHRONICLES: CHOZI LA BUZI



By Julius Jumah
Samahani sana wanangu.
Wanangu salamu.
Hizi ni salamu za dhati, za upendo.
Salamu zitokazo ndani na mvunguni mwa moyo wangu.
Salamu zilizobeba dhati ya nafsi yangu.
Salamu adimu kwenye ulimwengu tunamoishi.
Nisameheni wanangu.

Moyo umenituma........
Moyo wangu umenituma barua niwaandikie.
Nyie wana na vijana wangu.

Ikikufikia mweleze na mwenzako.
Mmmh mwanangu, niandikapo barua hii,
Najua mko mahala flani.

Ama ni asubuhi jasho likiwatiririka kwa kuangalia ponografi kwenye intanet kafee baada ya kutoroka shuleni.

Si ajabu kuwa ni usiku wa manane, mmegeuka kuwa bidhaa zinazotembea nusu uchi mkifukuzana na polisi, rambo mkononi wasijue mmefikaje pale.

Na pengine, licha ya umri wa miaka 12, mko leba mkisubiri ule wakati mchungu sauti ya muuguzi ikikwambia pipi ulimumunya peke ako.

Wanangu, pengine ni usiku katikati mko kwenye pati ya kucheza uchi ujira ni pakiti ya sigara.
Au labda mko shuleni chini ya miti mkisoma, mliopo kwenye vyumba mmejaa mithili ya siafu.
Yawezekana pia kuwa ninapoandika waraka huu mpo majalalani mkichakuachakua vifusi vya taka kama kuku wa kienyeji kutafuta makope ya kuchezea.

Ama mwacheza mpira wa makaratasi vichochoroni maana uwanja wenu umezungushwa mabati na kuandikwa "mbwa kali" kisha ujenzi wa kasino.

Walonyakua ardhi yenu ya shule ya Lang’ata bado wapo mamlakani wakiitwa ‘Private Developer’, walofuja mamilioni yenu zaidi ya mia saba bado wapo na kupigiwa upato kutwaa ugavana kaunti fulani.

Wanangu lakini pengine mmejikongoja hadi sekondari. Maisha ya manamba ndio staiki yenu, bila mikiki hakuna lishe.

Uchungu wa mwana aujuae mzazi
Wanangu, machozi yanitiririka kiwango cha kulowesha karatasi hii.
 Mniruhusu wanangu nkomee hapo, ntaendelea nafsi ikijikubali.

 (Asante sana nguli Mrisho Mpoto)




Ungana nami kwenye:
Facebook: Jumah Mlavidavi
FBPage: Kocha Mlavidavi Jumah
Twitter: @Jumah_Mlavidavi
Instagram: Jumah_Mlavidavi


No comments: